Abugida (kutoka Ge‘ez አቡጊዳ ’abugida) ni muundo wa mwandiko mwenye alama kwa silabi yaani konsonanti pamoja na vokali. Ni mwandiko wa kawaida kwa lugha za Ethiopia na Uhindi ya Kaskazini.
Jina latokana na herufi nne za kwanza ya mwandiko wa Ge'ez ambayo ni lugha ya kale ya Ethiopia.
Tofauti yake na alfabeti kama mwandiko wa Kilatini ni ya kwamba hapa kuna alama za pekee kwa vokali na konsonanti zinazounganishwa kufuatana na mahitaji ya lugha. Tofauti na miandiko ya abjadi kama Kiarabu au Kiebrania ni ya kwamba abjadi mara nyingi haziandiki vokali.
Kwa mfano wa mwandiko wa Devanagari ya Kihindi kuna alama ya क ambayo ni "k" na pia silabi "ka". Kwa kuongeza mstari mdogo juu silabi mpya ya के ke inapatikana. Ule mstari mdogo unaomaanisha "e" haupatikani peke yake bali pamoja na alama ya konsonanti pekee.
Kutoka alama ल "l" / "la" kuna uwezekano wa kupata alama kwa ला lā, लि li, ली lĪ, लु lu, लू lū, ले le, लै lai, लो lo na लौ lau.