Amri Kumi ni orodha ya amri kuu za Mungu katika Biblia. Za kwanza zinamhusu Mwenyezi Mungu mwenyewe, na zile zinazofuata mpaka mwisho zinahusu jirani, yaani binadamu wengine kuanzia wazazi.
Toleo la awali linapatikana katika kitabu cha Kutoka 20:1-17. Toleo la pili liko katika Kumbukumbu la Torati 5:1-21.
Amri hizi ni sehemu ya Torati ya Kiyahudi na kukubaliwa pia na Wakristo walio wengi kama amri zinazowahusu wao pia, tena wanaziona kuwa kimsingi zinawadai watu wote.
Hata hivyo wafuasi wa Yesu Kristo wanazishika kadiri ya utimilifu wake ulioletwa naye kama Agano Jipya. Mifano ya ukamilisho huo ni mafundisho ya Yesu katika Injili ya Mathayo 5:17-48.