Atanasi wa Aleksandria anayeitwa Mkuu (pia Athanasio (Kigir. Ἀϑανάσιος Athanasios; Aleksandria, Misri, 295 hivi - Aleksandria, 2 Mei 373) alikuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini Misri, mwanatheolojia mashuhuri aliyetetea mafundisho ya Utatu dhidi ya Uario na anayeheshimiwa kama Babu wa Kanisa. Wakopti wanamhesabu kama Papa wa 20 wa Aleksandria.
Chini ya makaisari mbalimbali, kuanzia Konstantino Mkuu hadi Valens, maisha yote ya Atanasi yalihusika na juhudi kubwa za Kanisa kwa ajili ya kufafanua na kutetea imani sahihi juu ya Yesu na juu ya Utatu hata akaitwa mapema “nguzo ya Kanisa” (Gregori wa Nazianzo) dhidi ya uzushi wa Ario. Kwa ajili hiyo alistahimili kwa ushujaa kupigwa vita na wafuasi wa huyo na viongozi wa serikali waliompeleka uhamishoni mara tano.
Kwa mafundisho yake na kwa upendo wake motomoto kwa Kristo, tangu zamani anaheshimiwa na Wakatoliki, Waorthodoksi na Waorthodoksi wa Mashariki kama mtakatifu na mmojawapo kati ya mababu wa Kanisa walio muhimu zaidi. Anakumbukwa pia katika kalenda ya Waanglikana na Walutheri.
Mwaka 1568 Papa Pius V alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.
Wote wanaadhimisha sikukuu yake kila mwaka tarehe 2 Mei[1].