Baisikeli (kwa kawaida baiskeli; pia basikeli; kutoka Kilatini "bis", "mara mbili" na Kigiriki "κύκλος", kyuklos, "duara" kupitia Kifaransa/Kiingereza "bicycle") ni chombo cha usafiri kinachoendeshwa kwa nguvu ya misuli ya binadamu.
Baisikeli huwa na magurudumu mawili yanayoshikwa na fremu, kiti kimoja, kanyagio, breki na usukani. Tabia nyingine za kawaida ni kuwa na taa mbele na nyuma. Baisikeli bora huwa pia na gia zinazorahisisha kazi ya kukanyaga kanyagio.
Kwa kawaida nguvu hupelekwa kwa nyororo kutoka kanyagio kwenda gurudumu la nyuma. Magurudumu huwa na matairi yaliyojaa hewa.
Katika nchi nyingi baisikeli ni chombo muhimu cha usafiri. Zamani baisikeli ilikuwa usafiri wa maskini lakini pia katika nchi kadhaa zilizoendelea watu hutumia baisikeli ama kwa usafiri wa mjini au kwa burudani.
Sayansi imegundua ya kwamba baisikeli ni usafiri wa haraka mjini katika umbali wa kilomita chache. Katika nchi nyingi kuna njia za pekee kwa ajili ya baisikeli kando ya barabara ya magari.
Baisikeli ni usafiri unaotumia nishati kidogo na hivyo kuwa nafuu kwa hifadhi ya mazingira.
Mashindano ya baisikeli ni tawi muhimu la michezo ya kimataifa.