Bikira Maria wa Lurdi (kwa Kifaransa: Notre Dame de Lourdes au Notre-Dame-de-Lourdes; kwa Kiingereza "Our Lady of Lourdes") ni jina mojawapo la Bikira Maria lililotokana na njozi maarufu zilizojirudia mwaka 1858 alizozisimulia Bernadeta Soubirous, msichana mnyenyekevu wa Lourdes, Ufaransa.
Binti huyo alisema kwamba aliwezeshwa kumuona mara kadhaa katika pango la Massabielle kati ya milima Pirenei kwenye mto Gave karibu na kijiji cha Lourdes.
Njozi hizo zilithibitishwa na Kanisa Katoliki kuwa za kuaminika, hata ikaanzishwa kumbukumbu yake katika liturujia kila tarehe 11 Februari, ilipotokea njozi ya kwanza[2]. Kutokana na wingi wa miujiza iliyowatokea wagonjwa wanaohiji huko kwa mamilioni, siku hiyo inaadhimishwa na Kanisa kama Siku ya Kimataifa ya Wagonjwa.