↑Maneno "Binadamu" na "Mwanadamu" ni maneno mawili yaliyo tofauti kimatamshi lakini yenye maana moja kidhana. Neno "Binadamu" kietimolojia huundwa na maneno mawili tofauti ambayo hutokana na lugha ya Kisemiti katika lahaja za Kiarabu na Kiebrania ambapo neno "Bin" etimolojia yake ni lugha ya Kiarabu ambapo neno hilo Bin humaanisha "Mtoto wa jinsia ya kiume". Halikadhalika neno "Adamu" etimolojia yake ni kutoka katika lugha ya Kiebrania ambapo neno hilo Adamu hutokana na neno "Adamah" lenye maana ya "Ardhi". Kwa upande mwingine neno "Mwanadamu" huundwa kutokana na etimolojia mbili tofauti kutoka katika lugha za Kiswahili na Kiebrania ambapo katika etimolojia ya lugha ya Kiswahili hutoka neno "Mwana" ambalo humaanisha "Mtoto" na ambapo pia etimolojia yake hutoka katika neno la Kibantu "Omona/Umwana" lenye maana ya "Mtoto wa jinsia ya kiume au kike". Hivyo basi, kietimolojia inaposemwa "Bin-Adamu" humaanishwa "Mtoto wa jinsia ya kiume wa kiumbe hai yeyote mwenye asili ya ardhi" yaani "Adamah", na halikadhalika inaposemwa "Mwana-Adamu" humaanishwa "Mtoto wa jinsia ya kiume au kike aliyetokana na kiumbe hai yeyote mwenye asili ya udongo".