Bunge

Chumba cha Wawakilishi katika Bunge la Australia.
Jumba la Westminster ni Bunge la Ufalme wa Muungano.

Bunge ni chombo cha kutunga sheria na pia ni mmoja wa mihimili mitatu inayounda mfumo wa utawala kulingana na mgawanyo wa madaraka katika dola. Mihimili mingine ni mahakama na serikali.

Bunge ni chombo kinachotokana na mfumo wa utawala wa Westminster, ambao umerithiwa na nchi nyingi duniani kutoka Uingereza. Kutokana na mfumo huo kuenea, mara nyingi Bunge la Uingereza huitwa "Mama wa Bunge" duniani.

Bunge la kwanza nchini Uingereza liliundwa wakati wa utawala wa Mfalme Henri III katika karne ya 13. Bunge hilo lina sehemu mbili, Bunge la Makabwela na Bunge la Mabwanyeye.

Katika nchi nyingi zinazofuata mfumo wa Westminster, Waziri Mkuu huwa ndio kiongozi mkuu wa serikali bungeni.

Shughuli za bunge husimamiwa na mbunge aliyechaguliwa kama mwenyekiti, rais au spika wa bunge.

Kuna aina mbili za bunge:

  • Bunge la "chumba kimoja" ambako wawakilishi wote wa wananchi hukaa na kufanya maazimio pamoja
  • Bunge la "vyumba viwili" ambako kitengo kikubwa zaidi kina kazi ya kutunga sheria na wabunge wake huchaguliwa moja kwa moja na wananchi katika majimbo ya uchaguzi yanayotakiwa kuwa takriban na idadi ya wapiga kura sawa. Kitengo kingine mara nyingi huitwa "senati" au "chumba cha juu" kwa kawaida ni kidogo zaidi, wabunge wake huchaguliwa ama na wawakilishi wa mikoa au majimbo au wanateuliwa pia kufuatana na kanuni za katiba (k.m. kwa shabaha ya kuwakilisha makundi maalumu katika jamii) na madaraka yake kwa kawaida ni madogo lakini inathibitisha au kukataa sheria zilizoamuliwa na bunge la kwanza; lakini hapa kuna tofauti nyingi kati ya nchi na nchi.[1]
  1. Kamusibunge kamusi bunge.

From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne