Chembeuzi za jinsia (pia: kromosomu za jinsia, ing. sex chromosomes) ni mbili kati ya chembeuzi za binadamu na za wanyama mbalimbali zinazoongoza utengenezaji wa seli zote za mwili kadiri ya urithi wa wazazi unaotunzwa katika DNA.
Hizo chembeuzi za jinsia kwa binadamu ni chembeuzi X na chembeuzi Y. Ndizo zinazosababisha mtu kuwa mwanamume au mwanamke, na vilevile wanyama mbalimbali kuwa wa kiume au wa kike.
Baba tu ana chembeuzi Y (pamoja na ile ya X) na hivyo anaweza kumrithisha mwanae, ambaye kwa njia hiyo atakuwa wa kiume.
Kumbe mama ana jozi la chembeuzi X asiweze kurithisha chembeuzi Y.
Ndiyo maana ni baba tu anayesababisha jinsia ya mtoto wao.