Damu (kutoka neno la Kiarabu) ni kiowevu katika mwili wa binadamu na wanyama. Inazunguka mwilini ndani ya mishipa ya damu ikisukumwa na moyo kwa lengo la kumwezesha kuishi.
Kazi ya tishu hiyo ni kupeleka lishe na oksijeni kwa seli za mwili na kutoa daioksaidi ya kaboni pamoja na uchafu mwingine kutoka seli.
Ndani ya damu kuna utegili (kwa Kiingereza plasma) ambao ni kiowevu chake pamoja na seli za damu nyekundu na nyeupe. Seli nyekundu hubeba oksijeni wakati daioksaidi ya kaboni hubebwa na utegili. Seli nyeupe ni kama walinzi wa mwili wa kupambana na magonjwa. Pia kuna chembe sahani.
Mtu mzima huwa na damu lita 6 mwilini.