Daudi (Biblia)

Daudi akimmaliza Goliathi katika mchoro wa Caravaggio.

Daudi (kwa Kiebrania דוד, Daud, kwa Kiarabu داوُد, Dāwūd; Bethlehemu, mnamo 1040 KK - Yerusalemu, 970 KK hivi) alikuwa mfalme wa pili wa Israeli ya Kale mnamo 1010 KK-970 KK. Alimfuata mfalme Sauli akafuatwa na Suleimani.

Mwana wa Yese, kama kijana alipelekwa kwenye jumba la mfalme Sauli alipopanda ngazi na kuwa kiongozi wa kijeshi.

Kati ya matendo yake yaliyokumbukwa zaidi, mojawapo ni ushindi juu ya Mfilisti Goliathi.

Alipata neema kwa Mungu akapakwa mafuta matakatifu na nabii Samueli ili atawale taifa la Israeli; alihamishia mjini Yerusalemu Sanduku la agano, na Bwana mwenyewe alimuapia kwamba uzao wake utadumu milele, kwa sababu kutoka kwake atazaliwa Yesu Kristo kadiri ya mwili [1].

Daudi alimuua mwanajeshi wake Uria na kumuoa mke wake Bathsheba: hivyo alifanya dhambi lakini Mungu alimtuma nabii wake Nathani kumlaumu. Daudi aliomba msamaha akasamehewa na Mungu.

Pamoja na makosa hayo na mengine, Daudi akabaki kielelezo cha mfalme wa Israeli, ambaye awe tofauti na watawala wengine wote kwa kuwa hasa mtumishi mnyenyekevu wa Mungu bila kuyumba kwa kuelekea miungu mingine.

Tangu kale anaheshimiwa kama mtakatifu tena nabii kutokana na Zaburi zake.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 29 Desemba[2].

  1. https://www.santiebeati.it/dettaglio/83350
  2. Martyrologium Romanum

From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne