Dhahabu | |
---|---|
Jina la Elementi | Dhahabu |
Alama | Au |
Namba atomia | 79 |
Uzani atomia | 106.42 u |
Valensi | 2, 8, 18, 32, 18, 1 |
Ugumu (Mohs) | 2.5 |
Kiwango cha kuyeyuka | 1337.33 K (1064.18 °C) |
Kiwango cha kuchemka | 3129 K (2856 °C) |
Dhahabu (kutoka Kiarabu ذهب, dhahab) ni elementi yenye namba atomia 79 katika mfumo radidia na uzani atomia ni 196.966569. Alama yake ni Au (kutoka Kilatini aurum).
Ni metali adimu nzito yenye rangi ya njano nyeupe hadi njano nyekundu. Kiwango chake cha kuyeyuka ni 1337.33 K (1064.18 °C). Dhahabu haiathiriwi kwa urahisi kikemia: hii ndiyo sababu ya kung'aa kwa miaka mingi, kwa kuwa haishikwi na kutu.
Ni kati ya metali za kwanza kutumiwa na wanadamu. Sababu kubwa ni kwamba dhahabu hupatikana kama metali tupu. Atomu zake haziungani na elementi nyingi kuwa molekyuli ya dutu mpya, hivyo dhahabu haiozi kwa kushikwa na kutu. Ni elementi chache zinazoweza kuathiri dhahabu, hasa halojeni kadhaa. Rangi yake ni ya kuvutia na tabia yake ya kuchongeka baridi kwa kuponda tu kuwa bati au waya inawezesha watu kuipa maumbo tofauti. Ni metali laini, haifai kwa silaha au vifaa vya kazi lakini ilitumiwa tangu zamani kwa mapambo au kwa vyombo vya thamani katika utumishi wa kidini au wa kifalme.