Diego Garcia

Mahali pa Diego Garcia
Kisiwa cha Diego Garcia kwa macho ya ndege

Diego Garcia ni atolli ya Kiingereza katika Bahari Hindi, kati ya Tanzania na Indonesia. Ni sehemu ya funguvisiwa la Chagos na leo kisiwa pekee chenye wakazi ambao ni wanajeshi wa Marekani. Ni kituo kikubwa cha kijeshi cha Marekani katika Bahari Hindi.

Kati ya miaka 1850 na 1965 kisiwa kilikuwa sehemu ya koloni la Morisi. Mwaka 1965 kilitengwa na Morisi pamoja na funguvisiwa lote. Mwaka 1971 Uingereza ilikodisha Diego Gracia kwa jeshi la Marekani ambao walitaka kuwa na kituo cha kijeshi kwenye Bahari Hindi katika mashindano yao na Umoja wa Kisovyeti.

Katika miaka miwili iliyofuata wenyeji wote wa funguvisiwa waliondolewa visiwani, wakahamishiwa na watoto wao huko Mauritius, Shelisheli na Uingereza. Wengi wao wanapigania haki ya kurudi. Mahakama ya Uingereza iliwaruhusu mwaka 2000 warudi tena lakini serikali imekataa mwaka 2004.

Diego Garcia ilikuwa kituo muhimu katika vita vya Marekani huko Afghanistan na Irak. Ndege za kijeshi za aina B-52 zinatoka hapa pamoja na ndege za kubeba petroli.

Marekani ina pia kituo cha manowari zake kisiwani.


From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne