Ekumeni ni tapo la Ukristo linalolenga kurudisha umoja kamili kati ya madhehebu yake mbalimbali.
Msingi wake ni imani inayowaunganisha katika Yesu Kristo na kwa njia yake katika Utatu mtakatifu, yaani Mungu pekee aliye Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.
Neno linatokana na Kigiriki oikouméne, linalomaanisha kwa asili sehemu ya dunia iliyokaliwa na watu; hivyo likaja kuwa na maana ya jambo linalohusu waamini duniani kote.
Ekumeni ilianza kati ya Waprotestanti, hasa lilipofanyika Kongamano la Kimisionari la Kimataifa huko Edimburg, mwaka 1910, ambapo waliohudhuria walisisitiza uhusiano kati ya umoja wa Wakristo na kazi ya uinjilishaji wa mataifa yote.
Mwaka 1937 iliundwa Halmashauri ya Kiekumeni ya Makanisa, ikijumlisha hata Waorthodoksi. Kwa sasa inawakilisha robo tu ya Wakristo wote, kwa sababu Wakatoliki na Wapentekoste wengi hawajajiunga na muundo huo.
Hata hivyo Kanisa Katoliki liliingia kwa nguvu katika juhudi za ekumeni kuanzia Papa Yohane XXIII (1958-1963) na Mtaguso wa pili wa Vatikano (1962-1965).