Mwaka wa liturujia |
---|
Magharibi |
Mashariki |
Epifania ni neno linatokana na Kigiriki ἐπιφάνεια, epifaneia, yaani udhihirishaji, tokeo, ujio, uwepo wa Mungu.
Kwa kifupi zaidi 'Eπιφάνια (Yohane Krisostomo) linamaanisha "Kuzaliwa kwa Yesu Kristo", kwa kuwa ndivyo Bwana alivyotutokea sisi binadamu kadiri ya imani ya Wakristo.
Kwa kawaida Epifania inaeleweka kama sikukuu muhimu mojawapo ya Ukristo ambayo inahusiana na Noeli na inaadhimishwa kimapokeo tarehe 6 Januari. Lakini, kuanzia mwaka 1970, Kanisa la Kilatini limeruhusu Wakatoliki wa nchi ambapo tarehe hiyo si sikukuu ya taifa, waiadhimishe katika Jumapili ya kwanza baada ya Januari mosi, isije ikasahaulika. Upande wao, Makanisa ya Kiorthodoksi yanayofuata bado Kalenda ya Juliasi wanaiadhimisha siku ambayo katika nchi nyingi ni tarehe 19 Januari, kutokana na tofauti ya siku 13 kati ya kalenda hiyo na ile ya Gregori.
Mbali ya kushiriki ibada kanisani, desturi zinazohusiana na Epifania ni pamoja na nyimbo maalumu, kuandika majina ya mamajusi katika milango kwa chaki, kubariki nyumba, kula keki ya mamajusi watatu, kuogelea na kuondoa mapambo ya Krismasi.