Falsafa (kutoka Kigiriki φιλοσοφία filosofia = filo, pendo la sofia, hekima) ni jaribio la kuelewa na kueleza ulimwengu kwa kutumia akili inayofuata hoja za mantiki. Kwa hiyo ili kutengeneza falsafa yako kunahitajika kuwa na hoja za msingi, hoja zilizojaa hoja (akili), kisha kuiweka falsafa yako kwa jamii ili waisome na kuielewa. Wapo watakaokubaliana na wewe kulingana na hoja zako na wapo watakaokupinga kutokana na hoja zako vilevile.
Falsafa huchunguza mambo kama kuweko na kutokuweko, ukweli, ujuzi, uzuri, mema na mabaya, lugha, haki na mengine yoyote.
Tofauti na dini, imani au itikadi, njia ya falsafa ni mantiki inayoeleza hatua zake ikiwa tayari kuchungulia upya kila hatua iliyochukua. Kwa hiyo falsafa ni njia ya kuuliza maswali na kutafuta majibu.
Katika lugha ya kila siku neno "falsafa" mara nyingi linachukuliwa kutaja jumla ya mafundisho au imani ya mtu au kundi la watu, kwa mfano "falsafa ya chama fulani", "falsafa ya maisha yangu" na kadhalika. Lakini kwa jumla fikra hizo hazistahili kuitwa "falsafa". Ila tu kuna makundi ya wanafalsafa wanaopendelea mielekeo tofauti na kuhusu haya inawezekana kutumia neno "falsafa ya fulani" kwa kutaja matokeo ya kazi yao.