Fonolojia (hasa huitwa Sarufi Matamshi) ni tawi la isimu yaani sayansi ya lugha. Inashughulikia uchunguzi na uchambuzi wa mfumo wa sauti ama matamshi ya lugha mahususi, kwa mfano ugawanyaji wa irabu na konsonanti za lugha ya Kiswahili. Hivyo fonolojia huchunguza sauti za lugha moja na matokeo yake yana umuhimu katika kubuni alfabeti ya kufaa kwa lugha husika.
Ala za sauti (vipashio vya utamkaji) zinatumika katika utamkaji wa fonimu (vitamkwa) za lugha husika. Mkondo wa hewa wakati wa utamkaji. Kuwepo na kutokuwepo kwa mguno wakati wa utamkaji (ghuna/sighuna).
Tawi hili la isimu hushughulikia kanuni zinazotawala uchambuzi wa mfumo wa sauti, yaani, sauti kutamkwaje na wapi katika kinywa cha mwanadamu.
Dhana ya fonolojia inajipambanua vizuri zaidi ikifasiliwa kwa kutofautishwa na fonetiki. Wakati fonetiki ni taaluma inayochunguza sauti zitamkwazo na binadamu bila kuzihusisha na lugha yoyote, fonolojia huchunguza mfumo wa sauti wa lugha mahususi kama vile sauti za Kiswahili, Kiingereza, Kimwera na Kinyaturu. Kwa ufupi, fonetiki huchunguza sauti zote zitamkwazo na binadamu; fonolojia huchunguza mfumo wa sauti wa lugha mahususi.
Hivyo, fonetiki huchunguza sauti nyingi kadiri iwezekanavyo, lakini fonolojia huchunguza sauti chache tu zilizomo katika mfumo wa sauti wa lugha husika. Mathalani, mfumo wa sauti wa lugha ya Kiswahili una sauti thelathini tu (irabu tano na konsonanti ishirini na tano).
Jambo lingine la kuzingatia ni vipashio vya kiuchambuzi vya matawi haya mawili. Wakati fonetiki kipashio chake cha msingi ni "foni", fonolojia kipashio chake cha msingi ni "fonimu". Kwa kuzingatia maelezo ya hapo awali, ni wazi kuwa foni ni nyingi zaidi kuliko fonimu, kwa kuwa foni ni kila sauti itamkwayo na binadamu, wakati fonimu ni sauti zile tu zilizomo katika mfumo wa sauti wa lugha mahususi. Hivyo, kuna fonimu za Kiswahili, za Kiingereza, za Kichina, n.k., lakini foni si za lugha yoyote, wala huwezi kusema kwa uhakika kuna foni ngapi, kwa kuwa bado kuna lugha nyingi duniani ambazo hazijatafitiwa.
Historia ya fonolojia inaweza kuwa imeanza na Ashtadhyayi, sarufi ya Kisanskrit iliyoandikwa na Pāṇini katika karne ya 4 KK. Kwa namna ya pekee Shiva Sutras, nyongeza ya Ashtadhyayi, inaorodhesha fonemi ya lugha hiyo, pamoja na kujadili mofolojia, sintaksia na semantiki.