Hali maada katika fizikia ni muundo jinsi maada hutokea katika hali mbalimbali, ama kama elementi (dutu tupu) au kama kampaundi (dutu za mchanganyiko).
Hali nne za maada ambazo huonekana katika maisha yetu ya kila siku ni mango, kiowevu, plasma na gesi.
Duniani kwa kawaida kuna hali tatu za maada:
Hali maada hutofautiana jinsi vipande vidogo ndani ya dutu yaani atomu au molekuli zake zahusiana.
Katika hali mango zinakaa pamoja kila atomu mahali pake. Tunasema: Dutu ni imara. Dutu katika hali hii ina umbo, mjao na uzani maalumu. Yaani maada katika hali ya mango huchukua ujazo na umbo lisilobadilika, pamoja na chembe zake ambazo ni atomu, molekuli na ioni zikiwa zimeshikamana kwa pamoja katika eneo moja.
Katika hali kiowevu atomu zina nafasi ya kuachana na kubadilishana mahali. Tunasema dutu ni kama majimaji. Dutu katika hali hii ina mjao na uzani maalumu lakini haina umbo. Kiowevu chakubali kila umbo la chombo kinamomwagwa. Maada katika hali ya kiowevu huwa na ujazo usiobadilika, lakini huwa na umbo linalobadilikabadilika kutokana na chombo ilichowekwa. Chembe zake ziko karibukaribu lakini ziko huru.
Katika hali ya gesi atomu hazishikwi pamoja, zaelea kwa mwendo huria. Atomu na molekuli za gesi huelekea kusambaa na kukalia nafasi yote ambamo zimewekwa. Dutu katika hali hii ina uzani lakini haina umbo wala mjao kamili. Maada katika hali ya gesi ina ujazo pamoja na umbo ambalo hubadilikabadilika, vyote vikijibadilisha ili kujaza chombo ilichowekwa. Chembe zake haziko karibukaribu wala kukaa mahali pamoja bali huwa huru zikizungukazunguka katika sehemu zilipowekwa.
Maada katika hali ya utegili huwa na umbo na ujazo unaobadilika na pia huwa na atomu zisizo na chaji pamoja na idadi kadha ya ioni na elektroni, zote zikiwa na uwezo wa kusogea kwa uhuru.