Herode Mkuu (73 KK hivi - 4 KK) ni jina la heshima linalotumika kumtajia mtu maarufu zaidi wa ukoo wa kifalme wa Yudea katika karne ya 1 KK, yaani Herode (kwa Kiebrania הוֹרְדוֹס, Hordos, kwa Kigiriki: Ἡρῴδης, Hērōdēs).[1][2][3][4][5]
Akiwa kwa asili mtu wa kabila la Waedomu upande wa baba na Myahudi upande wa mama, alitawala Yudea yote chini ya himaya ya Dola la Roma.
Mkatili hasa, aliua hata mke wake mmojawapo na watoto watatu.
Ingawa alifuata dini ya Uyahudi na kuanza kazi kubwa ya kupanua na kupamba hekalu la Yerusalemu, alizingatia zaidi ustaarabu wa Kigiriki na kuendeleza miji kipagani.
Ni maarufu zaidi kutokana na taarifa za Injili ya Mathayo kuhusu jinsi alivyopokea kutoka kwa Mamajusi habari ya kuzaliwa kwa Mfalme wa Wayahudi, Yesu. Kwa hofu yake aliposhindwa kumtambua mtoto huyo, aliagiza wauawe watoto wote wa kiume chini ya umri wa miaka 2.