Itale (pia: matale; kwa ing. granite) ni mwamba mgumu wenye asili ya kivolkeno.
Imetokea pale ambapo magma imepoa na kuganda. Ndani ya magma kuna madini mbalimbali na mengine yalianza kuganda mapema kuwa fuwele wakati wa kupoa zinazoonekana kama punjepunje ndani ya itale.
Itale ni sehemu kubwa ya ganda la dunia. Inatokea ndani ya ganda lakini kutokana na mwendo wa gandunia ndani ya ganda sehemu kubwa zimesukumwa juu na kuwa milima ya itale au pandikizi ya miamba tu.
Itale ni jiwe bora kwa ujenzi. Ni ngumu sana, hivyo kuta za itale ni imara kabisa. Kama itale inakatwa, kusuguliwa na kung'arishwa inapata uso wa kupendeza unaofaa kwa mapambo ya ukuta, sakafu au meza za kazi.
Kwa uchongaji sanamu ni jiwe gumu sana linaloleta matokeo ya kudumu.