Jenetikia (kutoka Kigiriki cha kale γενετικός, genetikos, neno ambalo tena linatokana na γένεσις, genesis, "asili"[1][2][3]) ni tawi la biolojia linalochunguza uritishano na mwachano wa viumbe hai.[4][5]
Kwa namna ya pekee imegundulika kwamba chembechembe zinazohifadhi taarifa za urithi wa viumbe hai zimo katika kiini cha kila seli yao kama nyuzinyuzi zinazoitwa kromosomu. Hizo zinabeba jeni kadhaa ambazo kila mojawapo inahusika na urithi wa tabia na umbile fulani kutoka kwa wazazi kwenda kwa kizazi kipya.
Ukweli kwamba viumbe hai hurithi sifa kutoka kwa wazazi wao umetumika tangu zamani za kale kuboresha mazao ya mimea na wanyama kwa njia ya uzalishaji teuzi.
Hata hivyo, sayansi ya kisasa ya jenetikia, ambayo inajaribu kuelewa utaratibu wa urithi, ilianza tu na kazi ya Gregor Mendel katikati ya karne ya 19.[6] Ingawa hakujua msingi halisi wa urithi, Mendel aliona kwamba viumbe hurithi sifa kupitia vitengo maalumu ambavyo sasa vinaitwa jeni.
Jeni hufanana na maeneo ndani ya DNA, molekuli inayoundwa na mlolongo wa aina nne tofauti za nyukleotidi. Mpangilio wa nyukleotidi hizo ndio maelezo ya kijeni ambayo viumbe huyarithi. Kwa kawaida DNA ina umbo la ncha mbili, ambazo kila moja ina nyukleotidi zinazokamilishana. Kila ncha inaweza kutumika kama kiolezo katika uumbaji wa ncha nyingine mpya: hii ndiyo njia halisi ya kutengeneza nakala za jeni ambazo zinaweza kurithiwa.
Mpangilio wa nyukleotidi katika jeni hutafsiriwa na seli ili kuzalisha mlolongo wa aminoasidi, hivyo kutengeneza protini; utaratibu wa aminoasidi katika protini hufanana na utaratibu wa nyukleotidi katika jeni. Uhusiano huo kati ya mpangilio wa nyukleotidi na mpangilio wa aminoasidi hujulikana kama kanuni ya maumbile. Aminoasidi zilizo katika protini huamua jinsi inavyojikunja katika umbo la pande tatu; kisha, utendaji kazi wa protini hiyo hutegemea muundo huo. Protini hutekeleza karibu majukumu yote yanayohitajika ili seli ziishi. Mabadiliko ya DNA katika jeni yanaweza kubadilisha aminoasidi za protini, na hivyo kubadilisha umbo lake na utendaji kazi wake: mabadiliko haya yanaweza kuwa na madhara makubwa katika seli na kwa kiumbe kwa jumla.
Ingawa jenetikia ina athari kubwa katika sura na tabia za kiumbe, matokeo ya mwisho yanategemea mchanganyiko wa jenetikia na mambo ambayo kiumbe anayapitia wakati wa uhai wake. Kwa mfano, ingawa jeni zinaweza kuamua ukubwa au udogo wa kiumbe, lishe na mambo mengine ambayo kiumbe hupitia baada ya kuzaliwa pia huwa na athari kubwa.
{{cite book}}
: External link in |chapterurl=
(help); More than one of |editor1-first=
na |editor-first=
specified (help); Unknown parameter |chapterurl=
ignored (|chapter-url=
suggested) (help)