Kijerumani (pia: Kidachi[1], kwa Kijerumani: Deutsch au (die) deutsche Sprache) ni lugha ya Kigermanik ya magharibi katika jamii ya lugha za Kihindi-Kiulaya.
Huzungumzwa hasa katika nchi za Ujerumani, Austria, Uswisi, Liechtenstein na Luxemburg.
Kuna pia wasemaji asilia katika nchi jirani za Ujerumani / Austria kama Ubelgiji, Uholanzi, Ufaransa, Denmark, Poland na Italia ya kaskazini. Nchi nyingi za Ulaya ya Mashariki zilikuwa na wasemaji wa Kijerumani lakini wengi walifukuzwa au kuondoka wakati wa vita kuu ya pili ya dunia; vikundi vimebaki hasa katika Hungaria, Romania, Uceki, Urusi na Kazakhstan.
Vikundi vidogo vya watu waliohamia katika karne za 19 na 20 wanaoendelea kutumia Kijerumani wako katika Amerika ya Kaskazini (Marekani, Kanada), Amerika Kusini (Brazil, Chile) na Afrika (hasa Namibia na Afrika Kusini).
Kijerumani huzungumzwa na watu milioni 100 katika Ulaya. Ni lugha ya pili katika Ulaya baada ya Kirusi kushinda Kifaransa na Kiingereza.