Lithi (Lithium) | |
---|---|
Jina la Elementi | Lithi (Lithium) |
Alama | Li |
Namba atomia | 3 |
Mfululizo safu | Metali alikali |
Uzani atomia | 6.941 |
Valensi | 1 |
Densiti | 0.534 |
Ugumu (Mohs) | 0.6 |
Kiwango cha kuyeyuka | 453.69 K (180.54 °C) |
Kiwango cha kuchemka | 1615 K (1342 °C) |
Asilimia za ganda la dunia | 0.006 % |
Hali maada | imara |
Lithi ni elementi na metali alikali yenye namba atomia 3 na uzani atomia 6.941 kwenye mfumo radidia. Alama yake ni Li. Jina linatokana na Kigiriki λίθος líthos "mwamba, jiwe" kwa sababu iligunduliwa mara ya kwanza ndani ya miamba.
Lithi ni elementi nyepesi kabisa kati ya elementi zote zilizo imara kwa hali ya kawaida. Inamenyuka haraka na maji, hivyo husababisha majeraha ikiguswa kwa mkono kwa sababu mmenyuko wake na unyevu wa ngozi.
Kwa asili haipatikani kama dutu sahili kwa sababu inamenyuka haraka kikemia lakini iko kwa kampaundi mbalimbali, hasa katika miamba ya itale. Lithi tupu inapatikana kwa njia ya kikemia na inaonekana kama metali nyepesi yenye rangi nyeupe-kifedha lakini haibaki hivyo kwa muda mrefu. Katika hewa yenye unyevu uso wake huwa haraka ganda la hidroksidi ya lithi yenye rangi ya kijivu. Kwenye hewa kavu uso huwa nitriti ya lithi yenye rangi kahawia. Kwa sababu ya mimenyuko hiyo ya haraka lithi ya kimetali hutunzwa ndani ya mafuta.
Matumizi yake ni ndani ya betri na katika dawa mbalimbali. Betri za kisasa zinazotumiwa katika simu za mkononi karibu zote zinatumia lithi. Mipango ya kutengeneza magari ya umeme inategemea betri za lithi na hivyo imetabiriwa ya kwamba bei yake itapanda.