Liturujia ya Milano ni liturujia maalumu ambayo inatumika katika sehemu kubwa ya jimbo kuu la Milano na katika parokia kadhaa za majimbo ya kandokando (Lecco, Como, Bergamo, Novara na Lodi) nchini Italia hadi baadhi ya zile za jimbo la Lugano (Uswisi).
Kesi ya pekee ni parokia ya Pescocostanzo iliyopo katika Italia ya kati inapotumika kwa ibada ya ubatizo.
Kama asili yake anatajwa babu wa Kanisa Ambrosi, aliyekuwa askofu wa jimbo hilo katika sehemu ya mwisho wa karne ya 4. Ndiyo sababu inaitwa pia Liturujia ya Ambrosi.
Baada ya Mtaguso wa pili wa Vatikano liturujia hiyo imeshughulikiwa sana na wachungaji na wataalamu mbalimbali hata kupata uhai mpya.
Ingawa Wakatoliki wa maeneo hayo (milioni 5 hivi) wanafuata liturujia hiyo, upande wa sheria za Kanisa hawatofautiani na wenzao wote wa Kanisa la Kilatini.