Liturujia ya Ugiriki

Undani wa Kanisa kuu la Utatu Mtakatifu, Chicago, Marekani.
Padri akiingia patakatifu akishika kitabu cha Injili.
Somo la Injili.
Litania ya wakatekumeni.
Padri akiingia patakatifu akibeba vipaji huku shemasi mdogo akishika chetezo.
Padri akisimama kwenye meza takatifu (altare).
Waamini wakijiandaa kupokea Ushirika mtakatifu.
Ugawaji wa Ushirika mtakatifu kwa waamini.
Askofu akifanya ishara ya msalaba kwa kitabu cha Injili juu ya kitambaa cha altare kiitwacho antimension.
Padri akiruhusu waamini kuondoka kwa msalaba wa baraka.

Liturujia ya Ugiriki, iliyoenea kutoka Konstantinopoli, sasa Istanbul (nchini Uturuki) ni liturujia ambayo lugha yake asili ni Kigiriki, lakini siku hizi inaadhimishwa katika lugha nyingine nyingi kukiwa na tofauti ndogondogo duniani kote.

Wanaoitumia hasa ni Waorthodoksi wote na baadhi ya Makanisa Katoliki ya Mashariki: hivyo ni ya pili kwa uenezi baada ya liturujia ya Roma.

Vitabu vyake vinaongoza Liturujia ya Kimungu (Ekaristi), Vipindi vya sala rasmi, Mafumbo matakatifu (Sakramenti) na sala, baraka na mazinguo mbalimbali, vilivyostawi katika Kanisa la Konstantinopoli.

Liturujia hiyo inahusika pia na namna maalumu za usanifu majengo, picha takatifu, muziki wa liturujia, mavazi na mapokeo zilizostawi vilevile karne hata karne kila ilikotumika.

Kwa kawaida mkusanyiko wa waamini huwa wamesimama muda wote wa ibada, na ukuta wa picha takatifu unaoitwa iconostasis unawatenganisha na patakatifu anapohudumia askofu au padri akisaidiwa na shemasi.

Ushiriki wa walei unajitokeza katika kusujudu mara nyingi na kuitikia sala na nyimbo.

Katika liturujia hiyo Biblia inatumika sana katika masomo na katika matini mengine vilevile.

Taratibu za saumu ni kali kuliko zile za Ukristo wa Magharibi na zinafuatwa katika vipindi vinne kwa mwaka: Kwaresima Kuu, Kwaresima ya Noeli, Mfungo wa Mitume na Mfungo wa Kulala kwa Bikira Maria. Pamoja na hayo, Jumatano na Ijumaa nyingi ni za kufunga chakula. Monasteri nyingi zina mfungo hata Jumatatu zote.


From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne