Lugha rasmi ni lugha iliyopewa cheo maalumu katika nchi fulani. Kwa kawaida ni lugha inayotumiwa hasa na serikali kwa mawasiliano kati ya ofisi zake na pia kwa matangazo rasmi, kwa mfano kwa kutangaza sheria. Ni pia lugha ya kuendesha kesi mahakamani na kuandika hukumu.
Kuna nchi zenye lugha rasmi moja tu lakini nchi nyingi huwa na lugha mbalimbali zinazokubaliwa kama lugha rasmi kwenye ngazi tofauti za serikali.
Katika nchi mbalimbali lugha rasmi imetajwa katika katiba ya taifa au katika sheria mahsusi, lakini nchi nyingine hazina sheria juu ya lugha rasmi hata kama hali halisi ipo na kueleweka.
Kwa mfano nchini Namibia Kiingereza ni lugha rasmi kufuatana na katiba lakini lugha kumi na moja nyingine (pamoja na Kiafrikaans na Kijerumani) zimetajwa kama lugha za taifa zinazoweza kutumiwa pia kama lugha ya kufundishia shuleni.
Nchi kadhaa zimekubali pia lugha ya alama jinsi inavyotumiwa na watu bubu kati ya lugha rasmi ya nchi.