Mageuko ya spishi

Mti wa uhai huonyesha mabadiliko wa spishi tangu mwanzo wa uhai

Mageuko ya spishi (kwa Kiingereza: evolution) ni nadharia ya kisayansi iliyobuniwa na kutumiwa na wataalamu wa biolojia, hasa tawi la jenetikia.

Inasema ya kwamba spishi za viumbehai zilizopo duniani leo zimetokana na spishi zilizokuwa tofauti za zamani.

Nadharia hii inategemea hoja ya kwamba awali uhai wote ulitokana na maumbo asilia.

Katika wazo hili spishi zote jinsi zilivyo sasa zinaendelea kubadilika kutoka mifumo rahisi ya maisha kuelekea mifumo kamili zaidi.

Mabadiliko hayo huonekana hasa pale ambapo viumbe vizalia huwa na sifa tofauti na zile za wazazi wao. Sifa hizi ni ishara za jeni ambazo hupitishwa kutoka kwa mzazi kwenda kwa watoto wakati wa uzazi. Tabia tofauti huwa zinapatikana ndani ya makundi ya viumbe kutokana na mabadiliko katika jeni za viumbe hao, mabadiliko ya maumbile na vyanzo vingine vya mabadiliko ya maumbile.

Mageuko hufanyika wakati michakato ya mageuko kama vile uteuzi wa asili (pamoja na uteuzi wa kijinsia) na mabadiliko makubwa ya mkondo wa jeni huchangia katika mabadiliko haya, na kusababisha tabia nyingine kuwa za kawaida au nadra katika kundi la viumbe hai. Ni mchakato huu wa mageuko ambao umetoa mabadiliko ya bioanuwai katika kila kiwango cha asasi ya biolojia, pamoja na viwango vya spishi, kiumbe mmojammoja na molekuli.

Msingi wa nadharia hii ni mabaki ya kisukuku ya viumbehai ambao hawapo tena duniani lakini wanafanana kiasi na viumbehai wa leo, pamoja na ulinganifu wa spishi za karibu na za mbali zaidi. Nadharia ya mageuko ya spishi inalenga kueleza mabadiliko hayo.

Leo hii ndiyo nadharia ya kibiolojia inayokubaliwa na wataalamu wengi hata kama kuna wapinzani kadhaa, hasa upande wa wenye imani kali ya dini, lakini pia wachache kwa sababu za kitaalamu.


From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne