Malaria

Protista ya plasmodium jinsi inavyoonekana kwa hadubini: ndiyo inayosababisha malaria

Malaria ni ugonjwa wa kuambukiza ambao unaenezwa na mbu wa jenasi Anopheles na kusababishwa na kidubini aina ya protisti Plasmodium.

Kutokana na uenezi wake katika nchi zinazotumia Kiswahili, mara nyingi ugonjwa huo huitwa "homa" tu, ingawa homa ni dalili yake mojawapo tu, pia kuna magonjwa mengi yanayosababisha homa.

Malaria inatokea katika maeneo ya kitropiki na yanayokaribia tropiki ikiwa ni pamoja na sehemu za Amerika, Asia na Afrika. Mwaka 2015 duniani kulikuwa na maambukizi milioni 214 ya malaria, [1] na watu 438,000 walikufa, wengi wao (90%) wakiwa barani Afrika, hasa watoto wachanga katika mataifa ya kusini kwa Sahara. [2]

Malaria ni mojawapo ya magonjwa yaliyoenea sana na ni tatizo kuu la afya ya umma. Kwa kawaida huhusishwa na umaskini, lakini pia ni sababu ya umaskini [3] na kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya uchumi.

Spishi tano za vimelea vya Plasmodium huweza kumwambukiza binadamu; aina iliyo mbaya zaidi husababishwa na Plasmodium falciparum. Malaria inayosababishwa na Plasmodium vivax, Plasmodium ovale na Plasmodium malariae husababisha ugonjwa usio shadidi sana kwa binadamu na aghalabu haijui. Spishi ya tano, Plasmodium knowlesi, husababisha malaria kwa nyani aina ya makaku lakini inaweza pia kumwambukiza binadamu. Kundi hilo la spishi za Plasmodium linalosababisha ugonjwa kwa binadamu hujulikana kama vimelea vya malaria.

Kwa kawaida, watu hupata ugonjwa wa malaria kwa kung'atwa na mbu wa kike wa jamii ya Anopheles aliyeambukizwa. Mbu aina ya Anopheles pekee ndio wanaoweza kusambaza malaria, na ni lazima wawe wameambukizwa kupitia damu waliyofyonza kutoka kwa mtu aliyeambukizwa. Mbu akimng'ata mtu aliyeambukizwa, huchukua kiasi kidogo cha damu: damu hiyo huwa na vimelea vya malaria. Wiki moja baadaye, wakati mbu anapofyonza mlo wake mwingine wa damu, vimelea hivyo huchanganyika na mate ya mbu na kuingia katika mfumo wa damu ya anayeng'atwa.

Vimelea hivyo huzaa ndani ya seli nyekundu za damu, na kusababisha dalili kama vile anemia, maumivu kidogo ya kichwa, shida ya kupumua, takikadia, n.k., aidha kuna dalili nyingine za jumla kama vile homa, baridi, kichefuchefu, mafua, na katika hali mbaya zaidi kupoteza fahamu na hata kifo.

Maambukizi ya malaria yanaweza kupunguzwa kwa kuzuia kung'atwa na mbu kutumia vyandarua, dawa za kuzuia wadudu, au hatua za kudhibiti maenezi ya mbu kama vile kunyunyizia dawa za kuua wadudu ndani ya nyumba na kupiga mifereji kuondoa maji yaliyosimama ambapo mbu hutaga mayai yao.

Majaribio yamefanywa kuibuka na chanjo ya malaria bila mafanikio makuu, pamoja na kuibua mbinu za udhibiti wa kiajabu zaidi, kama vile kubadili viini tete vya mbu ili kuwafanya sugu kwa vimelea pia umefikiriwa. [4] Ingawa utafiti unaendelea, hakuna chanjo iliyopatikana hadi sasa inayotoa ulinzi wa hali ya juu dhidi ya malaria [5]; mwaka 2015 ile pekee iliyoruhusiwa kutumika nje ya majaribio ni RTS,S, ambayo inatolewa kwa kudunga sindano mara nne, na hata hivyo ina ufanisi mdogo (26%-50%) kulingana na chanjo nyingine. Hivyo dawa za kuzuia lazima zitumiwe bila kukoma ili kupunguza hatari ya kuambukizwa. Madawa hayo ya kuzuia maambukizi mara nyingi huwa ghali mno kwa watu wengi wanaoishi katika maeneo ambapo ugonjwa huu hupatikana kwa wingi.

Watu wazima wengi wanaoishi katika maeneo ambayo ugonjwa huo umeenea huwa na maambukizi ya muda mrefu ambayo hujitokeza mara kwa mara, na pia huwa na kinga kidogo; kinga hiyo hupunguka kadiri muda unavyosonga; watu wazima kama hao wanaweza kuambukizwa malaria kali ikiwa wameishi muda mrefu katika maeneo ambapo ugonjwa huo haujaenea. Wanashauriwa kuchukua tahadhari kamili wanaporejea katika maeneo ambapo ugonjwa huo umeenea.

Maambukizi ya malaria hutibiwa kwa kutumia dawa ya malaria, kama vile kwinini au vizalika vya atemisinin. Hata hivyo, vimelea vimekuwa sugu kwa nyingi ya dawa hizo. Kwa hiyo, katika baadhi ya maeneo ya dunia, dawa chache tu ndizo zilizo na uwezo wa kutibu malaria kwa ufanisi.

  1. Malaria Facts. Centers for Disease Control and Prevention.
  2. "Malaria Fact sheet N°94". WHO. Retrieved 2 February 2016.
  3. "Malaria: Disease Impacts and Long-Run Income Differences" (PDF). Institute for the Study of Labor. Iliwekwa mnamo 2008-12-10.
  4. Yoshida S, Shimada Y, Kondoh D; na wenz. (2007). "Hemolytic C-type lectin CEL-III from sea cucumber expressed in transgenic mosquitoes impairs malaria parasite development". PLoS Pathog. 3 (12): e192. doi:10.1371/journal.ppat.0030192. PMID 18159942. {{cite journal}}: Explicit use of et al. in: |author= (help)CS1 maint: multiple names: authors list (link) CS1 maint: unflagged free DOI (link)
  5. "RTS,S vaccine protection rate". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2009-11-08. Iliwekwa mnamo 2009-11-19.

From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne