Manii (pia: shahawa[1]; kwa Kiing. sperm, spermatozoa) ni mbegu za madume wa wanyama zinazozalishwa katika korodani. Kila chembe ya manii (spermatozoo) ni seli inayoweza kusogea nje ya mwili.
Kazi yake ni kubeba kromosomu zenye taarifa za jenetikia (yaani sifa za mwili inakotoka) na kupitia uterasi ya jike na kuingia ndani ya virijaova (virija vya uzazi vya jike) huko ndani ya yai. Kuingia kwa spermatozoo ndani ya yai kunasababisha ungano la ADN ya yai na spermatozoo na mgawanyo wa yai ambalo ni chanzo cha kiumbehai mpya.
Umbo la spermatozoo linaundwa na "kichwa" kidogo kinachobeba ADN na mkia mrefu ambao mwendo wake unasogeza seli mbele. Umbo hilo linafanana na kiluwiluwi mdogo lakini ni seli 1 tu.
Manii ya binadamu huzalishwa katika korodani za mwanamume. Kila seli ya manii ina kromosomu 23. Seli za mwili huwa na kromosomu 46, kwa hiyo spermatozoo inabeba nusu ya taarifa zinazohitajika kwa kuanzisha kiumbe kipya. Nusu nyingine inapatikana katika yai la mwanamke ambako spermatozoo inaelekea kuingia.
Wakati wa tendo la ndoa manii yanachanganyika kwa viowevu kutoka kibofushahama na tezi za shahawa na mchanganyiko huo unafyatuliwa nje ya mboo. Kama hii inatokea ndani ya kuma ya mwanamke, shahawa inasambaa na kuenea ndani ya kuma. Ilhali idadi ya spermatozoo ni kubwa sana, yaani seli zaidi ya milioni mia nne (400,000,000), uwezekano ni mkubwa kwamba seli kadhaa zitafika hadi virijaova na kukuta yai lililo tayari. Si zaidi ya seli 100 kati ya milioni zilizotoka ambazo zinafika kwenye yai.[2]
Yai lililo tayari linapokea spermatozoo moja tu. Hapo kromosomu 23 ndani ya yai zinaunganishika na kromosomu 23 za spermatozoo na kufanya jumla ya 46 zinazotosha kuanzisha kiumbe kipya.