Mavazi

Kanga ni mavazi ya wanawake wa Afrika Mashariki (hapa: Pate).
Mwanamke akifua nguo zake

Mavazi (kutoka kitenzi "kuvaa") ni nguo ambazo huvaliwa na watu ili kufunika mwili au sehemu zake. Mavazi huwa na makusudi mbalimbali:

  • hukinga mwili dhidi ya baridi au jua kali pamoja na athira nyingine za mazingira zinazoweza kuathiri vibaya mwili uchi.
  • huwasilisha ujumbe kwa watu wengine kwa kuonyesha mtu fulani ni sehemu ya kundi (k.m. jeshi, timu, dini, kabila) au tabaka (nguo ghali za tajiri) au anapendelea jambo (nembo kwenye nguo).

Kimsingi nguo zinalingana na hali ya hewa na mazingira. Penye joto mavazi huwa mepesi na penye baridi huwa mazito zaidi. Kila utamaduni umebuni aina zake za mavazi.

Historia inaonyesha pia ya kwamba tangu kale tamaduni mbalimbali zimepokea mavazi kutoka nje na kubadilisha mitindo yao. Hata kama katika majira ya utandawazi watu wanavaa nguo zilezile bado wanaweza kuzitumia tofauti.

Kuna mavazi ya aina nyingi, kwa mfano ya kitambaa, nguo, sufi, ngozi au plastiki.

Vilevile mavazi hutofautishwa kama ni ya wanaume, wanawake au watoto, kama ni mavazi ya kikazi au ya nyumbani au ya sikukuu.

Tofauti nyingine ni kama mavazi ya chini au ya juu, au kama ni mavazi ya sehemu mbalimbali za mwili kama vile suruali, mashati, koti au viatu.

Utengenezaji na uuzaji ya mavazi ni sehemu muhimu ya biashara na kuna kazi nyingi zinazotegemea mavazi. Mavazi pia ni tasnia kubwa duniani inayohusisha ubunifu, uzalishaji, na mauzo ya nguo. Watu wanaweza kuchagua mavazi yao kulingana na mahitaji yao binafsi, muktadha wa kijamii, na mwenendo wa wakati huo.


From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne