Maziwa

Bilauri ya maziwa
Maziwa na asali
Mwanambuzi ananyonya maziwa

Maziwa ni kiowevu cheupe kinachotolewa na majike wa mamalia kama lishe kwa ajili ya watoto wao. Wanyama wadogo hulishwa maziwa katika miezi ya kwanza ya maisha yao hadi kuzoea chakula cha kawaida.

Nje ya lishe ya wanyama changa, maziwa hutumiwa na binadamu kama kinywaji na chakula. Watu hufuga wanyama wanaotoa maziwa, hasa ng'ombe, kwa kusudi la kukamua maziwa yao. Wanyama wengine wanaofugwa na kukamuliwa kwa maziwa yao ni mbuzi, kondoo na ngamia, farasi, punda na nyati.

Maziwa hunywewa au kuungwa katika upishi wa chakula. Tatizo la matumizi ya maziwa ni ya kwamba yanabadilika haraka. Inakamuliwa pamoja na vidubini ndani yake na pia vidubini vilivyomo hewani hupenda kuingia ndani yake kwa sababu maziwa yana lishe nyingi. Vidubini hivi vinasababisha kuchachuka kwa maziwa; mara nyingi ladha inaweza kubadilika kwa namna isiyotakiwa.

Kwa hiyo maziwa yanayotolewa kwenye viwanda vya maziwa hupata upasteurishaji na hutunzwa kwenye baridi chini ya kiwango cha 7°C. Katika mazingira asilia maziwa yaliyochachuka hunyewa au, kama yameganda, huliwa.

Katika nchi nyingi maziwa hugandishwa na kukaushwa kuwa jibini. Maziwa katika umbo la jibini hutunzwa muda mrefu na ni chakula bora. Njia nyingine ya kutunza maziwa ni kuondoa maji ndani yake kabisa na kutunza unga la maziwa.

Mafuta ya maziwa hutolewa mara nyingi kuwa krimu au siagi.


From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne