Miungu (wingi wa mungu) ni jina linalojumlisha wahusika wanaoabudiwa katika dini mbalimbali kama wenye nguvu na enzi juu ya maisha ya binadamu. Huogopwa kama Mwenyezi Mungu.
Jamii za Afrika zilikuwa na dini zao ambamo tunaweza kuona imani katika nguvu za kiroho ambazo zinaitwa majina tofauti. Tunaweza kukuta imani ya Mungu Mkuu, pia ya miungu mbalimbali, pamoja na imani ya kuwepo kwa roho za wahenga, mizimu na pepo mbalimbali.
Tukijiuliza juu ya uhusiano kati ya mizimu, roho, miungu mbalimbali na Mungu Mkuu, ni lazima kwanza tujue imani za jadi hutofautiana kutoka jamii moja hadi jamii nyingine.
Mara ningi imani za Kiafrika humwona Mungu Mkuu mmoja kuwa wa juu na mwenye nguvu zaidi. Yuko kabla ya kila kitu kingine na asili yake haijulikani. Hivyo nguvu hutazamwa kwa ngazi tofauti; Mwenyezi Mungu yuko juu, chini yake kuna roho mbalimbali au hata miungu pamoja na nguvu za asili, na mwishoni binadamu wasio na nguvu nyingi.
Wakati mwingine hadithi za uumbaji za Kiafrika zinamwonyesha Mungu akiwa au akienda mbali na watu au hawasiliani nao tena moja kwa moja. Anaacha washughulikiwe na roho au miungu midogo aliyoumba pia. Mungu wa aina hiyo anaonekana mbali sana na mambo ya binadamu; kwa sababu hiyo, mara kwa mara miungu midogo huombwa badala yake ili kupata usaidizi. Katika jamii nyingine wanaamini kwamba mizimu inaweza kuleta mawasiliano baina ya Mungu na binadamu.
Vikundi vingine humwona Mungu Mkuu kuwa karibu sawa na miungu mingine, kama mwenyekiti wao au kama mfalme kati ya machifu. Wafon katika Afrika ya Magharibi humwaza Mungu mkuu kama mapacha mawili: Mavu, nguvu ya kike, na Lisa, nguvu ya kiume. Wakitazamwa kama nguvu moja huitwa Mavu pekee. Wameumba watoto ambao hutawala shughuli za dunia na viumbe vyake kama miungu.
Dhana za aina hiyo zimeleta majadiliano kati ya wataalamu kuhusu kuainisha dini za Kiafrika kuwa za Mungu mmoja (monotheistic) au za miungu mingi (polytheistic). Wengine huona uainishaji huo hauna maana kwa dini za Kiafrika.
Mtaalamu John Mbiti wa Kenya aliona kwamba kimsingi imani katika Mungu mmoja inapatikana kwa namna moja au nyingine katika dini zote za asili. Anaeleza nguvu nyingine za kiroho kama tabia au shughuli za Mungu yeye yule zinazotazamwa pekepeke.
Kwa jumla katika utamaduni wa Kibantu kwa jumla hakuna wazo la miungu mingi. Katika mapokeo hayo Mungu ni mmoja tu, lakini kuwasiliana naye kulifanyika kwa njia ya mizimu hasa, si moja kwa moja. Hata hivyo katika maeneo kadhaa kulikuwa na wazo la kuwepo kwa pepo muhimu waliostahili ibada inayofanana na ile inayotolewa kwa miungu[1].
Katika sehemu nyingi za dunia utamaduni wa asili ulikuwa na imani ya miungu mingi, jinsi ilivyo katika sehemu nyingi za Afrika Magharibi. Imani hizo zilipatikana hata katika mazingira ya taifa la Israeli, na pia wakati alipoishi Yesu, ingawa Wayahudi walishika imani yao ya pekee.
Dini za miungu mingi (kwa Kiingereza: "polytheism") zilikuwa kawaida katika Afrika Kaskazini, Afrika Magharibi, Ulaya na sehemu nyingi za Asia kabla ya uenezaji wa Ukristo na Uislamu.
Kati ya miungu mingi iliyoabudiwa kila mmoja aliaminika kuwa na idara yake alipotawala hasa, kama vile hali ya hewa, vita, kifo, uponyaji, mavuno, mifugo, biashara, uzazi n.k.
Lugha ya Kiingereza inatunza mpaka leo kumbukumbu ya miungu mingi iliyoabudiwa katika utamaduni wa Ulaya wa Kale kabla ya kuingia kwa Ukristo. Majina ya siku za juma ni majina ya miungu ambayo siku ziliaminiwa kuwa chini ya ulinzi wao hasa.
Kumbe miungu iliyomaanisha nyota au sayari, kama vile Jua, Mwezi na Saturn ilikuwa mapokeo ya Roma, si asili ya Uingereza.