Mkate wa uzima (kwa Kigiriki ἄρτος τῆς ζωῆς, artos tēs zōēs) ni mojawapo kati ya namna saba ya Yesu Kristo kujitambulisha katika Injili ya Yohane kwa kutanguliza "Mimi ndimi..."[1].
Yesu alijiita hivi baada ya kuzidisha mkate na samaki kwa umati wa watu waliomfuata.
Lengo la muujiza huo halikuwa tu kutuliza njaa yao, bali kudokeza karamu ya mbinguni ambayo itashibisha hamu zote za binadamu kwa utimilifu wa uzima.
Hotuba hiyo inapatikana katika Yoh 6:22-59 ambamo imeandikwa kuwa ilitolewa katika sinagogi la Kapernaumu.[2]
Pamoja na kwamba Injili hiyo haisimulii jinsi Yesu alivyowaachia wanafunzi wake mwili na damu yake katika maumbo ya mkate na divai wakati wa karamu ya mwisho, inazungumzia fumbo la ekaristi hasa katika sehemu ya mwisho ya hotuba hiyo, ikisisitiza kuwa Yesu amejifanya chakula kweli na kinywaji kweli[3].
Kwa njia yake tu mtu anaweza kuwa na uzima wa Kimungu (Yoh 5:26)[4].