Msalaba ni ishara inayotokana na mistari miwili kukutana katikati yake.
Hiyo ni mojawapo kati ya ishara maarufu na ya zamani zaidi duniani kote, katika sanaa, utamaduni na dini, hasa Ukristo unaoheshimu kama ukumbusho wa kifodini cha mwanzilishi wake, Yesu Kristo, aliyekufa kwa njia ya usulubisho.
Msalaba ulikwishatumiwa na Wakristo wa kale sana. Mwanzoni mwa karne ya 3 Tertullianus, katika kitabu "De Corona", alisema kwamba walikuwa na desturi ya kujifanyia ishara hiyo katika paji la uso.
Lakini alama ya msalaba au za kufanana na msalaba zinapatikana pia katika tamaduni mbalimbali tangu kale bila uhusiano wowote na Ukristo.
Misalaba iliyotumiwa kwa adhabu ya kifo iliweza kuwa na maumbo mbalimbali, hata kuwa ubao mmoja tu bila mikono ya kando.