Msalaba wa Yesu ni msalaba ule ambao Yesu Kristo alisulubiwa juu yake hadi kifo chake kilichotokea huko Yerusalemu kwa amri ya Ponsyo Pilato siku ya Ijumaa, labda tarehe 7 Aprili 30 BK.
Tukio hilo, pamoja na ufufuko wa Yesu unaosadikiwa na Ukristo kutokea siku ya tatu (Jumapili ya Pasaka), ndiyo kiini cha imani ya dini hiyo mpya iliyotokana na ile ya Uyahudi.
Kwa Wakristo fumbo hilo la Pasaka ndilo kilele cha historia ya wokovu inayotangazwa na Biblia ya Kikristo.
Fumbo hilo lilisababisha kazi nyingi za sanaa ya Kikristo, hasa uchoraji na uchongaji.