Mwakanuru

Kuna nyota 33 ndani ya miaka 12.5 ya mwanga kutoka Jua

Mwakanuru (kwa Kiingereza: "Light year" ) ni kizio cha umbali kinachotumiwa katika fani ya astronomia. Ni kipimo cha umbali ambao mwanga umeusafiri kwa mwaka mmoja wa dunia yaani siku 365.25.[1].

Msingi wa kipimo hiki ni kasi ya nuru. Nuru inatembea takriban kilomita 300,000 kwa sekunde. Idadi kamili ni mita 299,792,458 kwa sekunde moja. Mwezi wa Dunia yetu una umbali na Dunia kama sekunde moja ya nuru au kilomita lakhi tatu na dunia.

Katika mwaka mmoja umbali huo unafika mita 9.461  × 1015.

Kipimo hiki kinahitajika kutaja umbali kati ya nyota za angani. Umbali huu umepimwa kuwa miakanuru mia, elfu au hata milioni kadhaa. Kutokana na ukubwa wa ulimwengu umbali katika anga-nje ni kubwa sana.

Hali halisi hatuoni nyota jinsi zilivyo "sasa" lakini jinsi zilivyokuwa wakati uliopita kutegemeana na umbali wao. Nyota jirani kabisa na jua letu inaitwa Alpha Centauri umbali wake ni 4.2 mwakanuru maana yake nuru yake inahitaji zaidi ya miaka minne hadi imefika kwetu. Kwa maana nyingine tunaiona nyota hii jinsi ilivyoonekana miaka minne iliyopita.

Tukiangalia nyota ambazo ziko mbali sana, nuru yake imesafiri miaka elfu kadhaa. Kwa darubini tunaona nyota ambazo nuru yake imeshapita miaka milioni kadhaa. Inawezekana kwamba nyota kadhaa tunazoona hazipo tena. Hasa tukizingatia nyota kubwa sana zilizo mbali uwezekano ni mkubwa kwamba zimelipuka tayari[2].

  1. Measuring the Universe The IAU and astronomical units, Tovuti ya Ukia, iliangaliwa Julai 2017
  2. How Many Stars In The Night Sky Still Exist?, tovuti ya Forbes, Aug 20, 2016

From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne