Mwinjili Luka (kwa Kigiriki Λουκᾶς, Lukas) ni Mkristo wa karne ya 1 ambaye tangu zamani za Mababu wa Kanisa anasadikiwa kuwa mwandishi wa Injili ndefu kuliko zote za Biblia ya Kikristo. Humo alisimulia kwa ufasaha na kupanga kwa utaratibu mzuri matendo na mafundisho ya Yesu, akastahili kuitwa "mwandishi wa upole wa Kristo" (Dante Alighieri)[1].
Vilevile anasadikiwa kuwa mwandishi wa kitabu cha Matendo ya Mitume kinachoendeleza Injili hiyo ili kuonyesha kazi ya Yesu Kristo ilivyoendelea katika Kanisa lake kwa nguvu ya Roho Mtakatifu hadi mwaka 63 BK.
Hivyo Luka, mtunzi pekee wa Agano Jipya asiye Myahudi, anahesabiwa kuwa ameandika robo ya sehemu hiyo ya pili ya Biblia nzima ya Ukristo.
Pamoja na Wakristo wengine wengi, Kanisa Katoliki linamheshimu kama mtakatifu na msimamizi wa madaktari hasa katika sikukuu yake, tarehe 18 Oktoba[2].