Ndoa

Pete, alama ya ndoa.

Ndoa ni muungano kati ya watu wawili au zaidi unaokubaliwa na kuheshimiwa na jamii. Tukio la kuanzisha ndoa linaitwa harusi, na kabla ya ndoa kuni kipindi cha uchumba ambapo watu hao wawili walio kubaliana wanachunguzana tabia na kujifunza au kujuana zaidi baina yao. Kama watu wanaohusika wakikomesha ndoa yao kisheria, hali hii inaitwa talaka.

Katika utamaduni wa nchi nyingi uhusiano huo ni kati ya mwanamume mmoja na mwanamke mmoja tu na unalenga ustawi wao na uzazi wa watoto katika familia.

Katika nchi nyingine, hasa za Kiislamu na za Afrika, inakubalika ndoa kati ya watu wawili ambao mmojawapo ana au anaweza kuwa na mwenzi au wenzi wengine pia (mitara au upali), hususan ndoa ya mwanamume mmoja na wanawake zaidi ya mmoja. Kumbe kwingine, hasa Ulaya, hilo ni kosa la jinai.

Mara nyingi harusi inafanyika kwa ibada maalumu kadiri ya dini ya wahusika.

Baadhi ya madhehebu ya Kikristo yanatazama ndoa kati ya wabatizwa wawili kuwa sakramenti: rejea Ndoa (sakramenti). Hasa Kanisa Katoliki linaamini ndoa haiwezi kuvunjwa kwa talaka kutokana na kauli ya Yesu: "Mungu alichokiunganisha, binadamu asikitenganishe" (Mk 10:9).


From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne