Papa Gregori I (Roma, Italia, takriban 540 – Roma, 12 Machi 604) alikuwa Papa kuanzia 3 Septemba 590 hadi kifo chake[1].
Alimfuata Papa Pelagio II akafuatwa na Papa Sabinian.
Jina lake la kuzaliwa pia lilikuwa Gregorius. Kutokana na umuhimu wake katika historia, hasa ya Kanisa na ya Italia, aliongezewa lile la Magnus, yaani "Mkuu".
Lakini mwenyewe, aliposikia kuwa Patriarki wa Konstantinopoli alijiita "Patriarki wa ekumene", aliitikia kwa kujiita "Servus servorum Dei" (yaani "Mtumishi wa watumishi wa Mungu"), jina linalotumiwa hata leo na kila Papa. Akijali umoja wa kidugu katika Kanisa lote, yeye aliona unyenyekevu unatakiwa kuwa adili la msingi la kila askofu kama lilivyokuwa kwa Kristo aliyetuosha miguu. Jina hilo alilojichagulia lilidhihirisha kabisa namna yake ya kuishi na kutenda.
Hamu yake ilikuwa kuishi kweli kama mmonaki, akizama daima katika Neno la Mungu, lakini kwa kumpenda alijifunza kuwa mtumishi wa wote katika nyakati za tabu.
Hivyo akawa mchungaji bora katika kuongoza Kanisa, katika kusaidia kwa hali na mali wenye shida, katika kustawisha maisha ya kimonaki na katika kuimarisha na kueneza kotekote imani, akiandika kwa ajili hiyo vitabu maarufu vya maadili na uchungaji[2].
Tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.
Mwaka 1298 Papa Bonifasi VIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.