Rastafari (wakati mwingine huitwa Urastafari) ni dini iliyoanzishwa huko Jamaika miaka ya 1930. Wakati mwingine dini hii hutambuliwa pia kuwa mfumo wa maisha na vuguvugu la kitamaduni.
Rastafari inarejelea imani zao, ambazo zinategemea ufafanuzi maalum wa Biblia, kama "Rastaloji". Msingi wake ni imani ya Mungu mmoja ambaye anajulikana kama Yahu (Jah) ambaye anaishi ndani ya kila mtu.
Mfalme wa zamani wa Ethiopia, Haile Selassie, anapewa umuhimu wa pekee. Marasta wengi humuona kama mwili wa Jah duniani na kama ujio wa pili wa Yesu Kristo. Wengine humwona kama nabii wa kibinadamu ambaye alitambua kikamilifu uungu wa ndani ya kila mtu.
Rastafari inatilia mkazo Afrika, na Afrika ya ughaibuni ambayo wanaamini kuwa inanyanyaswa ndani ya jamii ya Magharibi, au "Babeli". Marasta wengi wanasisitiza wito kwa Waafrika walioko nchi za magharibi wa kurudi Afrika, hasa Ethiopia. Wanaamini kuwa bara la Afrika ni Nchi ya Ahadi ya "Sayuni".
Marasta huita mfumo wao wa maisha "uhai" (livity). Ibada zao huita "misingi" (groundations), na hujumuisha muziki, kuimba, majadiliano na bangi, ambayo huonekana kama sakramenti.
Marasta wengi hula vyakula vya asili bila nyama wala chumvi (vyakula hivi huitwa itali), wanaacha nywele zao kukua bila kuchanwa au kukatwa (dreadlocks).
Inaaminika kuwa kuna wastani wa Rasta milioni 1 duniani.
Mmoja wa Rastafari maarufu sana duniani ni mfalme wa Rege, Bob Marley.