Sakramenti katika mapokeo na imani ya Ukristo ni ishara na chombo cha neema ya Mungu.
Jina hilo linatokana na neno la Kilatini "sacramentum" linalofanana na lile la Kigiriki "mysterion" (siri au fumbo) .
Ni mafumbo kwa kuwa ishara ya nje (vitendo na vitu vinavyosindikizwa na maneno maalumu) zinamletea mtu neema zisizoonekana.
Wakatoliki wanasadiki zina uwezo huo bila kutegemea utakatifu au sifa nyingine ya mhudumu anayezitoa kwa mwamini. Zinatenda "ex opere operato" (kwa Kilatini "kwa tendo kutendeka").
Kwa ajili hiyo ni lazima sakramenti ziwe zimewekwa na Yesu Kristo ambaye alizikabidhi kwa Kanisa ili liendeleze kazi yake ya kutakasa binadamu wote mahali kote na nyakati zote.