Sikukuu ya msalaba ni adhimisho la liturujia ya madhehebu mbalimbali ya Ukristo wa mashariki na vilevile ya Ukristo wa magharibi, ingawa tarehe zinatofautiana.
Sikukuu inaitwa kwa Kigiriki Ὕψωσις τοῦ Τιμίου καὶ Ζωοποιοῦ Σταυροῦ[1] ("Kuinuliwa kwa Msalaba wenye kuheshimiwa na kuleta uzima"), kwa Kirusi Воздвижение Креста Господня na kwa Kilatini Exaltatio Sanctae Crucis ("Kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu"). Walutheri na baadhi ya Waanglikana wanaiita Holy Cross Day ("Siku ya Msalaba Mtakatifu"), pengine Feast of the Glorious Cross ("Sikukuu ya Msalaba Mtukufu").
Lengo ni kutukuza chombo cha wokovu wa binadamu wote kilichotumiwa na Mungu kadiri ya imani ya dini hiyo, yaani Yesu Kristo aliyeuawa juu ya msalaba huko Yerusalemu mwaka 30 hivi.
Wakati Ijumaa Kuu inalenga zaidi mateso ya Yesu, Mwanakondoo wa Mungu aliyeondoa dhambi ya ulimwengu, sikukuu hiyo inashangilia utukufu wa fumbo hilo, ambalo Mtume Paulo alilitangaza kuwa fahari yake pekee (Gal 6:14).
Kabla yake, Yesu mwenyewe alizungumzia "kuinuliwa" kwake (Yoh 3:14-15), akimaanisha kuinuliwa msalabani na mbinguni vilevile. Hivyo alidokeza kwamba msalaba wake haukuwa aibu, bali hasa utukufu.