Sungusungu

Kuhusu wadudu wenye jina hili, tazama Sungusungu (sisimizi)

Sungusungu ni namna ya kutaja walinzi wa jadi nchini Tanzania. Asili yake ni vikundi vyao lilitokea katika jamii za Wasukuma katika Tanzania ya Magharibi.

Jina hilo lilianza kupata umaarufu tangu miaka ya 1980 kati ya Wasukuma [1] walioona matatizo ya wizi wa mifugo na ujambazi kwenye barabara baada ya vita vya Kagera na kurudi kwa wanajeshi wengi nchini kutoka Uganda.

Kufuatana na kumbukumbu ya wenyeji, walianzia Wilaya ya Msalala, kata ya Jana na baadaye kuzinduliwa rasmi kata ya Mwalugulu, mwaka 1982[2]. Baada ya kuona polisi haikuadhibu wezi wa mifugo na kuhisi kwamba viongozi kadhaa upande wa serikali walishirikiana nao, wananchi wa Jana waliunda kundi la vijana waliomchagua chifu kati yao na kuwinda wezi.

Harakati hiyo ilienea kwenye kata za jirani. Wezi na majambazi waliuawa mara nyingi lakini vijijini Wasungusungu waliendelea kuwaua pia watu walioshtakiwa kuwa wachawi. Baada ya polisi kuwatafuta viongozi na kuwakamata, Wasungusungu walipata kibali cha rais Julius Nyerere waweze kuendelea[3].

Kati ya Wasukuma kulikuwa na utaratibu wa Wasungusungu; walisimamiwa na "ntemi" wao aliyesaidiwa na makamu wake, "ntwale" na katibu. Chini yao yuko "Kamanda" anayeongoza vijana wanaokwenda kuwakamata wezi au washtakiwa. Wote walishauriana katika "bunge la Sungusungu".

Kutoka Usukuma mtindo wa Sungusungu uliendelea kusambaa kama chombo cha usalama kwa kusaidiwa na vyombo vya dola hadi kuenea juu ya asilimia 20 za Watanzania wote.[4]

Katika miaka ya baadaye mitindo ya ulinzi wa wakazi wa eneo wasio watumishi wa serikali lakini wanashirikiana na vyombo vya serikali imesambaa pia katika miji ya Tanzania[5].

  1. Leticia K. Nkonya, Rural Water Management in Africa: The Impact of Customary Institutions in Tanzania,Cambria Press 2008, ISBN-10: 1604975377, ISBN-13: 978-1604975376, uk. 128, online hapa
  2. Shindikilagi ya Sungusungu ilivyotumika kwa mauaji ‘Operesheni Tokomeza Ujangili’ Ilihifadhiwa 22 Machi 2017 kwenye Wayback Machine., taarifa ya Shija Felician, kwenye gazeti la Mwananchi, 28/12/2013
  3. Hervé Maupeu & Kimani Njogu, Songs and Politics in Eastern Africa, Mkuki Na Nyota Publishers 2007, ISBN-10: 9987449425, ISBN-13: 978-9987449422, online hapa
  4. Joseph F Donnermeyer, The Routledge International Handbook of Rural Criminology, 2016, uk. 411, ISBN-13: 978-1138799745, ISBN-10: 1138799742 online hapa
  5. https://www.ippmedia.com/sw/safu/tuimarishe-usalama-kwa-maboresho-ya-sungusungu

From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne