Tabakamwamba

Muundo wa Dunia: 1: Ganda la Dunia (kibahari 1a na kibara 1b unene km 0 hadi 80); 2: Koti la Dunia; 3: Kiini cha Dunia; 3a: Kiini cha nje (kiowevu); 3b: Kiini cha ndani (thabiti); 4: Tabakamwamba (ganda pamoja na sehemu ya juu ya koti); 5: Asthenosphere.
Faili:Upanuzi msingi bahari.PNG
Ganda la dunia, linaloitwa pia tabakamwamba, huonyeshwa kwenye picha kama mlia wa kijivu wa nje. Linakaa juu ya koti la dunia au tabakalaini ambalo ni magma au mwamba moto katika hali ya kiowevu kama uji. Ndani ya koti mna mizunguko ya mikondo ya mwamba moto kama ndani ya sufuria ambamo maji yanachemka. Katikati ya picha upande wa juu mkondo wa moto unasukuma ganda la nje. Unakata ganda na kusababisha kutokea kwa mabamba mawili yanayoachana polepole. Yanapoachana mgongo hujitokeza ambayo ni kama safu ya milima ya volkeno. Hapa magma kutoka koti hupanda juu na kupoa kuwa mwamba mpya. Mabamba mawili ya katikati yanayosukumwa na kupaa kwa magma hujisukuma chini ya mabamba jirani. Hapa kando ya bamba huelekea chini kungia katika tabakalaini ambako mwamba wake unayeyuka na kuwa magma tena.
Mabamba gandunia.

Tabakamwamba (kwa Kiingereza lithosphere)[1] ni sehemu thabiti ya nje ya sayari ya Dunia. Hiyo inamaanisha ganda la Dunia, pamoja na chini yake sehemu ya juu ya "koti la dunia". Tabakamwamba linakaa juu ya sehemu moto na laini ya ndani zaidi ya koti la Dunia.

Kwenye mpaka kati ya tabakamwamba na koti lenyewe liko tabaka kasiduni (ing. asthenosphere) ambayo ni nyumbufu kiasi.

Tabakamwamba linafanywa na miamba imara, tofauti na sehemu za ndani zaidi ya Dunia ambako mwamba na madini yote vinapatikana kwa hali nyumbufu au giligili kutokana na joto kali na shinikizo kubwa.

Eneo la tabakamwamba linagawiwa kwa vipande vikubwa ambavyo vinaelea juu ya sehemu moto za ndani. Vipande hivyo ni mabamba ya ganda la Dunia au kwa kifupi mabamba gandunia.

  1. IPA: lith'usfēr, kutoka maneno ya Kigiriki λίθος líthos (jiwe, mwamba) na σφαίρα sfaira (tufe, tabaka)

From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne