Thomas Aquinas Mtakatifu

Mchoro wake uliofanywa na Fra Bartolomeo
Mtakatifu Thoma wa Akwino
Mchoro wake uliofanywa na Carlo Crivelli.

Mtakatifu Thomas Aquinas (Roccasecca, katika eneo la watawala wa Aquino, leo katika wilaya ya Frosinone[1], Italia, 1224 au 1225 - Fossanova, wilaya ya Latina, Italia, 7 Machi 1274) alikuwa mtawa wa Shirika la Wahubiri na padri wa Kanisa Katoliki.

Mwenye akili kubwa ajabu, alishirikisha hekima yake ya pekee kwa mafundisho na kwa maandishi.

Mnyofu, mkimya, aliyekuwa tayari kutumikia, kiutu alipendwa na wote, naye alipendelea watu wa chini, akihubiria mafukara kwa usahili na wema hata zaidi ya mara moja kwa siku.

Kuliko wengine wote, Thoma aliona elimu na masomo kama njia ya kufikia utakatifu; ni kati ya watu bora upande wa nadharia, hasa wa teolojia ya shule, iliyofikia kilele chake katikati ya karne XIII.

Mwanafunzi wa Alberto Mkuu, alitumia hasa mawazo ya mwanafalsafa wa Ugiriki Aristoteli na ya Waarabu waliomtafsiri, lakini pia ya Plato: ili kufafanua imani, alikubali ukweli ulioweza kutolewa na yeyote, kwa sababu kweli zote zinatoka kwa Mungu; kinyume chake alikanusha udanganyifu wowote.

Hivyo aliweza kufanya usanisi mpana ambao mpaka leo Kanisa Katoliki linautambua kama tokeo bora la mafundisho yake lenyewe na kama kielelezo cha namna ya kufikiri na ya kufanya teolojia.

Anajulikana hasa kwa vitabu vyake “Jumla ya Teolojia” (kwa Kilatini Summa theologiae) na “Jumla dhidi ya Wapagani” (kwa Kilatini Summa contra gentiles).

Alitangazwa na Papa Yohane XXII kuwa mtakatifu tarehe 18 Julai 1323, halafu na Papa Pius V kuwa mwalimu wa Kanisa mwaka 1568. Kwa Kilatini anaitwa Doctor Angelicus (Mwalimu wa Kimalaika) au Doctor Communis (Mwalimu wa wote).

Ni msimamizi wa wanateolojia, wanachuo, watoaji na wauzaji wa vitabu, wanafunzi na shule.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 28 Januari[2].

  1. Wachache wanataja ngome ya familia katika mji wa Belcastro, karibu na Catanzaro, huko Calabria. Fiore, Giovanni (1999). Della Calabria illustrata (kwa Kiitaliano). Rubbettino Editore. ISBN 978-88-498-0196-5. Barrio, Gabriele (1571). De antiquitate et situ Calabriae (kwa Kilatini).
  2. Martyrologium Romanum

From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne