Trigonometria (kutoka Kigiriki trigonon = pembetatu na metron = kipimo, upimaji) ni sehemu ya jiometria, hivyo ni tawi la hisabati.
Inatazama habari za pembetatu na uhusiano kati ya pande na pembe. Uhusiano kati ya urefu wa pande na ukubwa wa pembe hufuata kanuni fulani na kwa kujua kanuni hizo inawezekana kukadiria umbali wa kitu au ukubwa la eneo kwa kujua habari chache tu.
Elimu hiyo ilitokea wakati wa utamaduni wa Ugiriki ya Kale wakati wataalamu walifanya utafiti wa nyota na kukadiria umbali wa nyota na dunia. Walitambua kanuni za trigonometria kwa mfano wa pembetatu mraba. Ilhali kila pembetatu inaweza kugawiwa kwa pembetatu mraba mbili, elimu hiyo inatosha kujibu maswali mengi.
Kwa kawaida trigonometria inatazama maumbo bapa lakini kuna pia trigonometria ya tufe, yaani kuangalia pembetatu zilizopo usoni wa tufe au mpira.