Uhuru wa dini

Hali ya uhuru wa dini nchi kwa nchi (Pew Research Center study, 2009). Rangi ya njano hafifu inamaanisha vizuio ni vichache, kumbe nyekundu inaonyesha kuna vizuio vingi.

Uhuru wa dini ni mojawapo kati ya haki za msingi za kila binadamu kutokana na hadhi yake inayomtofautisha na wanyama. Yaani akili yake inamfanya atafute ukweli, jambo linalohitaji kuwa huru kutoka kwa mwingine yeyote.

Uhuru huo unaendana na wajibu na haki ya kufuata dhamiri hasa katika masuala ya dini na maadili.

Haki hiyo inatajwa katika Tamko la kimataifa la haki za binadamu lililotolewa na Umoja wa Mataifa mwaka 1948, ingawa haitekelezwi vizuri katika nchi nyingi, hasa zile zinazofuata rasmi dini fulani au zinapinga dini zote.

Haki hiyo inajumlisha haki ya kuwa au kutokuwa na imani fulani, kuibadili, kuitekeleza katika ibada za binafsi na za pamoja, kuishuhudia kwa maneno na matendo, kuitangaza, n.k. maadamu mtu hatendi makosa ya jinai wala hasababishi vurugu katika maisha ya jamii.


From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne