Ukristo

Sanamu ya Kristo mkombozi huko Rio de Janeiro (Brazil) ni sanamu ya Yesu kubwa kuliko zote zilizopata kutengenezwa.


Ukristo (kutoka neno la Kigiriki Χριστός, Khristos, ambalo linatafsiri lile la Kiebrania מָשִׁיחַ, Māšîăḥ, linalomaanisha "Mpakwamafuta" [1]) ni dini inayomwamini Mungu pekee[2] kama alivyofunuliwa kwa Waisraeli katika historia ya wokovu ya Agano la Kale na hasa Yesu Kristo katika Agano Jipya ambaye ni mwanzilishi wake katika karne ya 1.

Dini hiyo, iliyotokana na ile ya Wayahudi, inalenga kuenea kwa binadamu wote, na kwa sasa ni kubwa kuliko zote duniani,[3][4][5] ikiwa na wafuasi 2,400,000,000 (33% kati ya watu 7.274 bilioni)[6][7][8][9], ambao nusu ni waamini wa Kanisa Katoliki na nusu ya pili wamegawanyika kati ya Waorthodoksi (11.9%) na Waprotestanti (38%) wa madhehebu mengi sana.

Karibu wote wanakubali Utatu Mtakatifu, yaani kwamba milele yote Mungu ni nafsi tatu zenye umoja kamili: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Ni kwa jina lao kwamba mataifa yote wanahimizwa kubatizwa kwa maji, ili kuzaliwa upya, kadiri ya agizo la Yesu ili kuingizwa katika fumbo la Mungu pekee kupitia fumbo la kifo na ufufuko wake mwenyewe.

Kitabu kitakatifu cha Ukristo kinajulikana kama Biblia. Ndani yake inategemea hasa Injili na vitabu vingine vya Agano Jipya.

Wakati wa Mababu wa Kanisa misingi ya imani ya Ukristo ilifafanuliwa na Mitaguso ya kiekumeni namna inayokubaliwa na wengi kabisa kati ya Wakristo wa leo. Maungamo yao yanakiri kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu aliyefanyika mtu ili kuwaokoa binadamu. Baada ya kuteswa na kuuawa msalabani alizikwa ila akafufuka, siku ya tatu akapaa kwa Mungu akishiriki mamlaka ya Baba hadi atakaporudi kuhukumu waadilifu na wasiotubu, akiwapa tuzo au adhabu ya milele kadiri ya imani na matendo yao.

Hivyo, kati ya madhehebu ya Ukristo, karibu yote yanamkiri Yesu kuwa kwa pamoja Mungu kweli na mtu kweli: katika umoja na nafsi yake ya Kimungu zinapatikana sasa hali hizo zote mbili.

Yote yanamkiri kuwa Mwokozi wa watu wote, na kuwa ndiye atakayerudi mwishoni mwa dunia kwa hukumu ya wote, ingawa maelezo kuhusu jambo hilo yanatofautiana.

Vilevile yote yanamchukua kama kielelezo cha utakatifu ambacho - kwa msaada wa Roho Mtakatifu na wa sakramenti zilizowekwa na Yesu mwenyewe, kuanzia ile ya ubatizo - kiwaongoze ndani ya Kanisa katika maadili yao maalumu, kuanzia unyenyekevu na upole hadi upendo unaowaenea wote, bila kumbagua yeyote, hata adui.

  1. Neno "Mkristo" (Χριστιανός) lilitumika mara ya kwanza kuhusiana na wafuasi wa Yesu katika mji wa Antiokia [Mdo 11:26] mwaka 44 BK. Wenyewe walikuwa wanajiita "ndugu", "waamini", "wateule", "watakatifu". Katika mazingira ya Kisemiti waliendelea na bado wanaendelea kuitwa "Manasara", yaani "Wanazareti" kutokana na jina la kijiji alikokulia Yesu. Kumbukumbu ya kwanza ya mwandishi ya neno "Ukristo" (Χριστιανισμός) ni katika barua za Ignas wa Antiokia, mwaka 100 hivi. See Elwell/Comfort. Tyndale Bible Dictionary, pp. 266, 828.
  2. Taz. Catholic Encyclopedia (article "Monotheism"); William F. Albright, From the Stone Age to Christianity; H. Richard Niebuhr; About.com, Monotheistic Religion resources; Kirsch, God Against the Gods; Woodhead, An Introduction to Christianity; The Columbia Electronic Encyclopedia Monotheism; The New Dictionary of Cultural Literacy, monotheism; New Dictionary of Theology, Paul, pp. 496–99; Meconi. "Pagan Monotheism in Late Antiquity". p. 111f.
  3. Hinnells, The Routledge Companion to the Study of Religion, p. 441.
  4. Zoll, Rachel (Desemba 19, 2011). "Study: Christian population shifts from Europe". Associated Press. Iliwekwa mnamo 25 Februari 2012.{{cite news}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  5. "The Global Religious Landscape: Christianity" (PDF). Pew Research Center. Desemba 2012. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2015-09-24. Iliwekwa mnamo 2012-07-30.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  6. 33.39% of ~7.2 billion world population (under the section 'People') "World". CIA world facts. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2010-01-05. Iliwekwa mnamo 2015-07-09. {{cite web}}: Unknown parameter |= ignored (help)
  7. "Christianity 2015: Religious Diversity and Personal Contact" (PDF). gordonconwell.edu. Januari 2015. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2017-05-25. Iliwekwa mnamo 2015-05-29. {{cite web}}: Unknown parameter |= ignored (help)CS1 maint: date auto-translated (link)
  8. "Major Religions Ranked by Size". Adherents.com. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2013-06-22. Iliwekwa mnamo 2009-05-05. {{cite web}}: Unknown parameter |= ignored (help)
  9. ANALYSIS (2011-12-19). "Global Christianity". Pewforum.org. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2018-12-26. Iliwekwa mnamo 2012-08-17. {{cite web}}: Unknown parameter |dead-url= ignored (|url-status= suggested) (help)

From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne