Ukuta wa Berlin (kwa Kijerumani Berliner Mauer) ulitenganisha sehemu mbili za jiji la Berlin (Ujerumani) kuanzia 13 Agosti 1961 hadi 9 Novemba 1989. Ukuta huo ulikuwa na urefu wa kilomita 45.3 ukiwa sehemu ya mpaka kati ya madola mawili ya Ujerumani yaliyokuwepo kuanzia 1949 hadi 1990. Ukuta wa Berlin ulikuwa mfano uliojulikana zaidi wa "pazia la chuma" katika Ulaya lililotenganisha nchi za kikomunisti za Ulaya mashariki na nchi za Ulaya magharibi. Takriban watu 200 waliuawa walipojaribu kuvuka ukuta kutoka mashariki kwenda magharibi.