Urundi (kwa tahajia ya Kifaransa pia Ouroundi) ni jina la kihistoria kwa nchi ya Burundi. Wajerumani waliita nchi "Urundi" walipoanza kueneza utawala wao juu ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.
Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia eneo hili lilivamiwa na jeshi la Ubelgiji kutoka koloni la Kongo ya Kibelgiji na kuwa eneo la kudhaminiwa chini ya Ubelgiji baadaye. Wabelgiji wakaitawala pamoja na Rwanda kwa jina la "Ruanda-Urundi" hadi uhuru kwenye mwaka 1962 na tangu wakati ule nchi inaitwa rasmi "Burundi".
Inaonekana ya kwamba Wajerumani walipoanza kutumia umbo la "Urundi" walifuata kawaida ya lugha ya Kiswahili badala ya jina la wenyewe ambapo silabi kwa mahali ni "Bu-" si "U-" jinsi ilivyo kwa Kiswahili.