Kitabu cha Waamuzi ni cha saba katika orodha ya vitabu vya Tanakh (Biblia ya Kiebrania) na vya Agano la Kale katika Biblia ya Kikristo.
Kinaleta mapokeo mbalimbali kuhusu historia ya Israeli kwenye miaka 1200-1025 hivi K.K.
Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.
Baada ya makabila 12 ya Waisraeli kugawana nchi takatifu, kila moja likaanza kujitegemea: lakini bila ya umoja hakuna nguvu upande wa dini wala wa siasa.
Upande wa dini, Waisraeli wakaanza kuchanganyikana na wenyeji Wapagani na kufuata utamaduni wao uliostaarabika zaidi, hata wakaabudu miungu yao kwa ukahaba wa kidini na kwa kuitolea sadaka watoto wao.
Kutokana na makosa hayo, Mungu akawaacha wanyanyaswe na makabila mbalimbali.
Mara kwa mara Waisraeli wakamlilia, naye akawainulia mwanamume au mwanamke fulani awashinde maadui na kuwarudishia amani (Amu 2:6-19).
Watu wa namna hiyo wanaitwa “waamuzi” kwa maana ya “watawala”. Majina yao ni: Othniel, Ehud, Shamgar, Debora, Gideoni, Tola, Yair, Yefta, Ibsan, Elon, Abdon, Samsoni.
Habari za waamuzi hao 12 haziwezi kupangwa kitarehe, kwa kuwa hazina dalili zinazotusaidia kujua ipi ilitangulia na ipi ilifuata. Waandishi wenyewe hawakujua mwaka wa matukio hayo, hivyo walikusanya kumbukumbu walizokuwanazo kama kwamba waamuzi walifuatana mmoja baada ya mwingine kuongoza Israeli. Ukweli ni kwamba waliweza kuongoza kwa wakati mmoja huyu huku na huyu huku, kwa kuwa kila mmoja alihusika na eneo fulani tu. Kwa kuwapanga mmoja baada ya mwingine, waandishi waliweza kusisitiza mara 12 kwamba Waisraeli walirudiarudia dhambi, na kwa sababu hiyo walirudiarudia kupewa na Mungu adhabu aliyoitabiri Musa. Lakini fundisho muhimu zaidi ni kwamba Bwana, bila ya kujali ugeugeu wao, daima alikuwa tayari kuwaokoa walipomlilia msaada.